IQNA

Kukamatwa jasusi wa Israel aliyemuua mwanasayansi wa Palestina

19:57 - January 11, 2022
Habari ID: 3474795
TEHRAN (IQNA)- Mashirika ya usalama ya harakati za kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza yamefanikiwa kumnasa mmoja wa wahusika wa mauaji ya kigaidi ya msomi na mwanasayansi wa Kipalestina aliyeuliwa huko Malaysia.

Fadi al Batsh mwanasayansi wa Kipalestina (kwenye picha) aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi Aprili 21 mwaka 2018 huko Kuala Lumpur Malaysia akiwa msikitini alikokwenda kwa ajili ya swala ya alfajiri. Dakta Fadi al Batsh alikamilisha kozi ya shahada ya kwanza na ile ya uzamili mwaka 2009 katika fani ya uhandishi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Ghaza. Baadaye alikubaliwa kujiunga na shahada ya uzamivu katika fani hiyo hiyo ya uhandisi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Malaysia. Mwanasayansi al Batsh ni kati ya watu wa kwanza waliowasilisha mpango wa kuasisi Umoja wa Kimataifa wa Wahandisi wa Palestina ili kuwa na mwakilishi huko Malaysia. Shahidi Fadi al Batsh aidha alikuwa Imam wa msikiti wa al Abbas; na alikuwa akifanya kazi katika taasisi ya masuala ya kheri kwa jina la "My Care" nchini Malaysia. Taasisi nyingi zinazojihusisha na masuala ya kujitolea ni matawi ya Taasisi ya My Care. 

Sababu za kuuawa Shahidi al Batsh

Baada ya kuuliwa Dakta al Batsh, Ahmad Zahid Hamidi Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo wa Malaysia alisema: 'Wauaji wa mhadhiri huyu aliyekuwa akifundisha katika Chuo Kikuu cha Kuala Lumpur Malaysia walikuwa na uhusiano na idara moja ya kijasusi ya nje ya nchi.' Kuhusu jinai hiyo, harakati na shakhsia mbalimbali wa Palestina pia walitangaza kuwa utawala wa Kizayuni ndio ulihusika na mauaji hayo ya kigaidi ya mwanasayansi wa Palestina. 

Ni wazi kuwa, kuna sababu kuu mbili kuhusu kuuliwa shahidi Fadi al Batsh. Sababu moja inahusiana na elimu aliyokuwa nayo msomi huyo wa Kipalestina kwa sababu Dakta Fadi al Batsh alikuwa mtaalamu wa uundaji wa makombora na ndege zisizo na rubani (droni). Sababu nyingine pia inahusiana na shughuli za kijamii alizokuwa akizifanya za kuunga mkono malengo ya Palestina. Utawala wa Kizayuni kamwe haukuafiki shughuli za kijamii za msomi huyo wa Kipalestina hasa zile za kuiunga mkono Palestina na kwa msingi huo ukaamua kumuua kigaidi mwanasayansi huyo wa Kipalestina. 

Mauaji ya kigaidi ya Dakta al Batsh yalikuwa muendelezo wa silsila ya hatua za kigaidi za utawala haramu wa Kizayuni. Ibrahim al Mad'hun mchambuzi wa masuala ya Palestina anasema: "Mauaji hayo ni katika muendelezo wa mauaji ya shakhsia wa Kiarabu na Kipalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni; na utawala ghasibu wa Kizayuni una rekodi ya kufanya mauaji mengi ya kigaidi dhidi ya shakhsia mbalimbali na jambo hilo si la kushangaza."

Kukamatwa mhusika wa ugaidi, kushindwa intelijensia ya Israel

Mhusika wa mauaji ya kigaidi ya al-Batsh alikamatwa kupitia operesheni kali ya kiusalama. Vyombo vya usalama vya mapambano ya Kiislamu ya Palestina vilifanikiwa kumnasa mhusika huyo wa ugaidi huko katika Ukanda wa Gaza baada ya kusikiliza kwa muda mrefu mazungumzo yake ya simu. Operesheni hiyo inathibitisha wazi kwamba vyombo vya intelijensia vya mapambano ya Kiislamu muda mrefu nyuma vilikuwa vimetambua na kumfuatiliwa kwa karibu mhusika wa mauji ya al-Batsh, jambo ambalo linathibitisha wazi uwezo mkubwa wa kiintelijensia na kiusalama wa harakati ya mapambano na vile vile kushindwa kiintelijensia utawala ghasibu wa Israel.

Mossad na ugaidi wa mara kwa mara

Suala jingine lenye umuhimu ni kwamba mhusika amekiri kwamba alitekeleza ugaidi huo kwa amri ya shirika la ujasusi la Israel, Mossad. Shirika hilo lina rekodi nyeusi katika kuwaua kigaidi wasomi, wawe ni wa Paletina au mataifa mengine. Muhammad az-Zawari ni mmoja wa wasomi ambaye aliuliwa na Mossad mwezi Disemba 2016 huko Tunisia kwa hoja kuwa alikuwa akitengeneza ndege zisizokuwa na rubani, droni.

Suala jingine muhimu ni kwamba utawala wa kigaidi wa Israel hujichukulia sheria mkononi na kuwaua kigaidi wasomi wa Kiislamu na Kiarabu bila kujali lolote kutokana na ukweli kuwa huwa haufuatiliwi kisheria kimataifa na kuwa una uungaji mkono na hulindwa na kutetewa na madola ya kibeberu duniani.

/4027347

captcha