IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Kupitia Siku ya Quds, wananchi wa Iran wametayarisha uwanja wa harakati kubwa ya Umma wa Kiislamu

18:23 - April 28, 2023
Habari ID: 3476927
TEHRAN (IQNA)- Imam wa Sala ya Ijumaa wa ya Tehran amesema kwamba wananchi wa Iran walichukua hatua madhubuti na kubwa kuelekea katika kuliwezesha zaidi taifa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, na ametoa shukrani zake kwa ushiriki mkubwa wa wananchi katika maandamano ya siku hiyo ya kuwaunga mkono mapambano ya ukombozi ya Wapalestina.

Katika khutba za Sala ya Ijumaa mjini Tehran, Hujjatul-Islam Wal Muslimin Hassan Abu Turabi Fard amesema: Kupitia hamasa yao kubwa katika Siku ya Kimataifa ya Quds, wananchi wa Iran wametayarisha uwanja wa harakati kubwa ya Umma wa Kiislamu na kudhihirisha uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina walio imara, washindi na wastahimilivu na wamepiga hatua madhubuti za kuongeza nguvu za Umma wa Kiislamu.

Imam wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amepongeza mahudhuria makubwa ya wananchi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuwataka kudumisha umoja na mshikamano na kubatilisha njama za adui anayefanya mikakati ya kuzusha hitiilafu baina ya Waislamu. 

Mamilioni ya wananchi wa Iran ya Kiislamu ​​walishiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuunga mkono mapambano ya ukombozi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuonyesha kuchukizwa kwao na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake hususan Marekani.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran yalihudhuriwa pia na maafisa wa serikali na jeshi chini ya kaulimbiu: “Palestina ni Mhimili wa Umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu; Quds Inakaribia Kukombolewa". Maandamano makubwa ya Siku ya Quds pia yalifanyika katika miji na vijiji zaidi ya elfu moja nchini Iran, sambamba na maeneo mengine ya dunia.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu yaliakisiwa na zaidi ya waandishi wa habari na wapiga picha 4,000, wanaowakilisha mashirika 150 ya habari ya ndani na nje ya nchi.  

Waislamu na wapenda haki kote duniani wamekuwa wakifanya maandamano kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds, na kuonyesha hasira zao dhidi ya siasa za kibaguzi za Israel na mshikamano wao na wananchi madhulumu wa Palestina.

4136969

captcha