IQNA

Zilzala Syria na Uturuki

Zilzala Syria na Uturuki: Idadi ya waliofariki dunia yafika 25,000, UN yatabiri itaongezeka maradufu

19:59 - February 11, 2023
Habari ID: 3476547
TEHRAN (IQNA)-Matumaini ya kupata manusura zaidi chini ya vifusi vya nyumba zilizobomolewa mitetemeko miwili mikubwa ya ardhi Jumatatu iliyopita katika nchi za Syria na Uturuki yanazidi kupungua siku 5 baada ya maafa hayo ambapo idadi ya walipoteza maisha hadi sasa ikifika 25,000 huku Umoja wa Mataifa ukitabiri kuwa yamkini idadi hiyo ikaongezeka maradufu.

Tetemeko la kwanza la  ardhi la ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Rishta lilitikisa kusini mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria Jumatatu asubuhi ya tarehe 6 Februari.  Kitovu chake kilikuwa ni katika mji wa Gaziantep wa Uturuki ambapo mamia ya majengo yameporomoka.Masaa machache baadaye kulijiri mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa 7.6 kwenye kipimo cha rishta.

Ingawa idadi kubwa zaidi ya wahanga wa mitetemeko hiyo imerikodiwa nchini Uturuki, lakini indhari zinazidi kutolewa kuhusu idadi ya vifo kaskazini mwa Syria, kutokana na uwezo mdogo, uhaba wa nyenzo, na kuchelewa kuwasili misaada ya kimataifa inayohitajika kwa shughuli za utafutaji na uokoaji wa watu walionasa chini ya vifusi.

Wakati huo huo, akizungumza katika mji wa Adana uliokumbwa na mitetemeko ya ardhi nchini Uturuki, Martin Griffiths alisema anatarajia makumi ya maelfu ya vifo kuthibitishwa. Griffiths, mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, alisema: "Nadhani ni vigumu kukadiria kwa usahihi idadi ya waliopoteza masiha kwani tunahitaji kuingia chini ya vifusi lakini nina uhakika itaongezeka maradufu au zaidi.

Huku matumaini ya watu waliokwama chini ya mabaki ya Uturuki na Syria yakififia, Griffiths alisema juhudi za uokoaji sasa ziko katika hatua za mwisho. Ameongeza kuwa, "Wanasema saa 72 ni kipindi cha dhahabu (kwa uokoaji)."

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi ametangaza kuwa watu milioni 5.3 wamepoteza makazi yao nchini Syria kutokana na tetemeko la ardhi la siku chache zilizopita na kwamba wanahitajia makazi kwa sasa.

Vilevile afisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema, tetemeko la ardhi la Syria linaweza kuitwa janga la ulimwengu lililosahaulika.

Wakati huo huo Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametaja hali ya Syria baada ya matetemeko la ardhi ya Jumatatu iliyopita kuwa ni ya maafa. 

Stephane Dujarric amesema kwamba vikwazo vya nchi za Magharibi havipaswi kuzuia misaada ya kibinadamu kutumwa kwa wahitaji nchini Syria, na Umoja wa Mataifa hautaki kuona suala la misaada inayohitajika nchini Syria likifanywa la kisiasa.

4121380

captcha