IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Matukio ya sasa Palestina yanaashiria kubatilishwa mipango yote ya mapatano na utawala wa Kizayuni

21:39 - April 29, 2022
Habari ID: 3475185
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema, Palestina nzima imekuwa uwanja wa mapambano, na kwamba mipango yote ya suluhu na kufanya mapatano na adui Mzayuni imebatilishwa.

Leo Ijumaa tarehe 29 Aprili 2022 inasadifiana na tarehe 27 Ramadhani 1443 Hijria, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Quds.

Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Quds kutokana na hatua ya Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ili Waislamu kote duniani waweze kutangaza hasira na kuchukizwa kwao na siasa za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu na kibla cha kwanza cha Waislamu.  

Katika hotuba yake iliyotangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya ndani na kimataifa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja dalili zenye kutia matumaini za mustakbali tofauti kwa ajili ya wananchi wa Palestina, ikiwa ni pamoja na kupanuka uwanja wa mapambano katika ardhi yote ya Palestina na kudhoofika utawala ghasibu na muungaji mkono wake mkuu yaani Marekani, na kusema kuwa, matukio ya hivi karibuni ya Palestina yana maana ya kubatilishwa mipango yote ya mapatano na utawala wa Kizayuni. Amekumbusha baraka zisizo na kifani za muqawama na mapambano katika eneo la Magharibi mwa Asia na kusisitiza kuwa: Masuala ya ulimwengu wa Kiislamu hususan kadhia ya Palestina hayaweza kutatuliwa isipokuwa kwa mapambano na muqawama.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba madhali utawala ghasibu na mtenda jinai wa Israel unaendelea kuikalia Quds kwa mabavu, kila siku ya mwaka inapaswa kutambuliwa kuwa ni Siku ya Quds. Amesema: Quds Tukufu ni moyo wa Palestina, na nchi yote iliyonyakuliwa ya Palestina kuanzia Bahari ya Mediterania hadi Mto Jordan ni mwendelezo wa Quds.

Amepongeza kusimama kidete na ujasiri usio na kifani wa wananchi wa Palestina na kuzitaja operesheni za kujitolea mhanga za vijana wa Kipalestina kuwa ni ngao ya ulinzi kwa Palestina inayotoa bishara ya mustakbali tofauti. Ayatullah Khamenei amesema: "Leo hii, irada isiyoweza kushindwa" huko Palestina na katika eneo lote la Asia Magharibi imechukua nafasi ya "jeshi eti lisiloshindwa" la Kizayuni; hivyo jeshi la wahalifu limelazimika kubadili safu yake ya ushambuliaji kuwa safu ya kujihami."

Ayatullah Khamenei ameendelea kuashiria mifano madhubuti ya kupanuka mapambano na muqawama katika eneo lote la Palestina, kama vile harakati ya kambi ya Jenin iliyowatia wazimu Wazayuni, wito wa asilimia 70 ya Wapalestina kwa ajili ya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya utawala ghasibu, harakati za kijihadi za Wapalestina katika maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa ardhi zilizoghusubiwa mwaka 1948, maandamano makubwa huko Jordan na Quds Mashariki (Jerusalem), hatua ya vijana wa Kipalestina ya kuulinda vikali Msikiti wa Al-Aqsa na mazoezi ya kijeshi huko Gaza na kusema: Palestina nzima imekuwa uwanja wa mapambano dhidi ya Wazayuni, na wananchi wa Palestina wana mtazamo mmoja kuhusu suala la kuendelezwa Jihadi.

Amesisitiza kuwa: Matukio haya muhimu yana maana ya utayarifu kamili wa Wapalestina wa kukabiliana na utawala ghasibu, na yanayaruhusu makundi ya Mujahidina kuingia katika medani ya vita wakati wowote mwafaka.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ujumbe muhimu wa matukio hayo na yaliyojiri Palestina katika miaka ya hivi karibuni ni kubatilishwa mipango yote ya mapatano na adui Mzayuni. Amesema: "Hakuna mpango wowote kuhusu Palestina unaoweza kutekelezwa bila kuwepo au kinyume na maoni ya wamiliki wake halisi yaani Wapalestina; hii ina maana kwamba, mikataba yote ya awali kama ule wa Oslo, au mpango wa kuundwa nchi mbili wa Kiarabu, au Muamala wa Karne, au kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kwa sura ya kudhalilisha kulikoshuhudiwa siku za karibuni, vimebatilishwa na kufeli."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinai za kila aina zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni licha ya kuonekana kuchoka na kuongeza kuwa: Wanaodai kutetea haki za binadamu wa Ulaya na Marekani ambao walizusha makelele mengi kuhusiana na kadhia ya Ukraine, wamenyamaza kimya mbele ya jinai zinazofanyika huko Palestina na wala hawawatetei watu wanaodhulumiwa, bali kinyume chake wanamsaidia mbwa mwitu mwenye kiu ya damu. 

Ayatullah Khamenei amelitaja somo kubwa la mwenendo huo wa udanganyifu wa madola ya kibaguzi ya Magharibi kuwa ni kuepuka kuyategemea madola hayo na kuongeza kuwa: Matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu, na zaidi ya yote, suala la Palestina, hayaweza kutatuliwa isipokuwa kwa nguvu ya muqawama na mapambano inayotokana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na sheria za Uislamu.

4053497

captcha