IQNA

Semina ya Nabii Isa AS katika Qur'ani yafanyika Kenya

12:09 - December 31, 2020
Habari ID: 3473510
TEHRAN (IQNA) – Semina ya Nabii Isa Masih, yaani Yesu, -Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-imefanyika nchini Kenya katika fremu ya 'Mazungumzo Baina ya Dini'.

Semina hiyo iliyofanyika Jumanne 24 Disemba iliandaliwa kwa ushirikiano wa Kituo cha Utamadni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Narobi na viongozi wa Kiislamu na Kikristo nchini humo.

Lengo la semina hiyo, iliyofanyika katika Ubalozi wa Iran mjini Nairobi, imetajwa kuwa ni kustawisha mshikamano na maelewano baina ya Waislamu na Wakristo nchini Kenya.

Akizungumza katika semina hiyo, Balozi wa Iran nchini Kenya Dkt. Jaafar Barmaki ameashiria kuishi kwa maelewano wafuasi wa dini mbali mbali nchini Iran na kusema, utulivu na amani ni dharura katika kuwepo usalama endelevu.

Dkt. Barmaki amazungumzia namna Uislamu unavyolipa umuhimu suala la wanadamu kuishi kwa maelewano ambapo ametoa mfano wa hilo kwa kuashiria Aya ya 13 ya Sura Hujurat katika Qur'ani Tukufu isemayo. "  Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari."

Akizungumza katika kikao hicho Bishop David Thagana Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kiinjilisti ya Kenya (FEICCK) alifafanua kuhusu maisha ya Nabii Isa AS na umuhimu wa kuwepo mazungumzo baina ya dini.

Naye Sheikh Yusuf Abu Hamza, Mkuu wa Masuala ya Kidini katika Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM) amezungumza katika semina hiyo na kusema Waislamu Kenya wanaishi kwa maelewano na wafuasi wa dini zinginezo nchini umo.

Kwa upande wake, Sheikh Mahdi Qassim, Imam wa Msikiti wa Mashia wa Park Road mjini Nairobi ameashiria aya za Qur'ani Tukufu kumhusu Nabii Isa AS. Amesema Nabii huyo mtukufu alileta amani na matumaini.

Kaimu mkuu Kituo cha Utamadni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Nairobi Bw. Abu Dhar Toghani amesema faili ya semina hiyo inaweza kupatikana katika ukurasa wa Instagram wa kituo hicho katika anuani ya https://www.instagram.com/iran.kenya

3944341/

captcha