IQNA

Aghalabu ya Waturuki wanataka Jumba la Makumbusho la Hagia Sophia liwe Msikiti tena

23:53 - June 12, 2020
Habari ID: 3472859
TEHRAN (IQNA) - Zaidi ya asilimia 73 ya watu wa Uturuki wanataka Jumba la Makumbusho la Hagia Sophia mjini Istanbul lirejee katika hadhi yake ya msikiti.

Kwa mujibu wa gazeti la Yeni Safak, uchunguzi wa maoni umebaini kuwa asilimia 73 wanataka jumbe hilo liwe msikiti huku watu wengine asilimia 22 wakipinga na asilimia 4.3 hawakuwa na maoni kuhusu kadhia hiyo.
Uchunguzi huo wa maoni ulifanyika Juni 2-5 2020 punde baada ya maadhimisho ya mwaka wa 567 tokea Utawala wa Uthmaniya uchukue udhibiti wa mji wa Istanbul. Aidha uchunguzi huo wa maoni umefanyika baada ya hafla maalumu ya kusoma Qur'ani Tukufu ndani ya Hagia Sophia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema kadhia ya Hagia Sophia si ya kimataifa bali inahusu mamlaka ya kujitawala. Kutokana na kuwa Hagia Sophia imesajiliwa na UNESCO kama turathi ya kimataifa, Uturuki itahitaji idhini ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa .
Jengo la Hagia Sophia ambalo baadhi ya wanahistoria wamelitaja kuwa miongoni mwa maajabu ya dunia ni kati ya maeneo yanayotembelewa zaidi duniani kutokana na vivutio vyake vya sanaa na usanifu majengo.
Jengo la Hagia Sophia lilijengwa mwaka 537 Miladia (CE) na lilipata umaarufu kutokana na kuba lake adhimu na wakati huo lilikuwa jengo kubwa zaidi duniani. Tokea mwaka 537 hadi 1453 lilikuwa ni Kanisa la Mashariki la Kiothodoxi na makao makuu ya Kasisi Mkuu wa Constantinople. Kwa muda mfupi, kati yaani kati ya mwaka 1204 hadi 1261, jengo hilo liligeuzwa na Wapiganaji wa Nne wa Msalaba kuwa Kanisa Katoliki. Wakati watawala wa silsila ya Wauthmaniya (Ottomans) walipouteka mji huo, mnamo mwaka 1453 Fatih Sultan Mehmet aliagiza jengo la Hagia Sophia litumike kama msikiti. Hadhi hiyo ya Hagia Sophia kama msikiti iliendelea kwa muda wa miaka 482 hadi mwaka 1935 wakati muasisi wa Jamhuri ya Uturuki, Mustafa Kemal Ataturk alipoagiza ligeuzwe na kuwa jengo la makumbusho.

/3471893/

captcha