IQNA

Ahadi ya Kweli

Hali ni shwari baada ya Iran kutungua quadcopter tatu katika mji wa Isfahan

18:02 - April 19, 2024
Habari ID: 3478703
IQNA-Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran umetungua ndege tatu ndogo zisizo na rubani aina ya quadcopter katika mkoa wa Isfahan ulioko katikati mwa nchi saa kadha baada ya vyombo vya habari vya Marekani kuwanukuu maafisa waandamizi wa nchi hiyo wakidai kwamba makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel yamepiga eneo la Iran.

Hata hivyo vyombo hivyo vya habari vimemnukuu Brigedia Jenerali wa Pili Siavash Mihandoust, afisa mkuu wa kijeshi mkoani Isfahan, akiviambia vyombo vya habari vya hapa nchini kwamba betri za ulinzi wa anga ziligonga "kitu kinachotiliwa shaka" na hakukuwa na uharibifu wowote uliotokea.

Isfahan NI mji muhimu kimkakati ukiwa na vituo muhimu kadhaa, ikiwa ni pamoja na vya utafiti wa kijeshi na vya maendeleo, pamoja na vituo vya kijeshi. Mji wa karibu na mkoa huo wa Natanz ni moja ya maeneo ya kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani ya nyuklia.

Vyombo vha habari vimebaini kuwa, mitambo ya ulinzi wa anga ya miji ya Isfahan na Tabriz iliwashwa kufuatia kuonekana vyombo vidogo kadhaa vya angani na vitu vya kutiliwa shaka.

Licha ya baadhi ya ripoti zilizodai kutokea miripuko katika miji hiyo, vyanzo vya kuaminika vimesema hakuna ripoti kwamba umetokea mripuko au kupigwa kwa kombora. Taarifa zaidi zimeeleza kuwa hali katika miji hiyo wakati huu ni shwari.

Awali mapema Ijumaa taarifa zilisambaa katika mitandao ya kijamii na kudai kuwa utawala haramu wa Israel umetekeleza mashambulizi ya makombora ndani ya maeneo kadhaa Iran. Sasa imebainika kuwa droni hizo ndogo aina ya quadcopter zilirushwa kutoka ndani ya Iran na watu wasiojulikana.

Ikumbukwe kuwa Aprili Mosi utawala wa Kizayuni ulifanya shambulizi la kigaidi dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus, mji mkuu wa Syria, na kupelekea kuuawa shahidi washauri saba wa kijeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC)  ambao walikuwa nchini Syria kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo. Katika kujibu jinai hiyo mapema Jumapili tarehe 14 April 2024 Iran ilifanya mashambulizi ya moja kwa moja ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Israel.

Operesheni hiyo ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyopewa jina la Ahadi ya Kweli ilikuwa haki yake ya kimsingi ya kujilinda, ambayo imeelezwa wazi chini ya Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa na katika kukabiliana na uchokozi wa kijeshi wa mara kwa mara wa utawala wa Israel, hasa mashambulizi ya kijeshi ya utawala huo dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran, mashambulizi ambayo ni kinyume kabisa cha kifungu cha 2 ibara ya 4 ya hati hiyo.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Meja Jenerali Hossein Salami ameuonya utawala wa Israel kwamba jibu la Iran litakuwa "kali zaidi" ikiwa utawala huo utatoa jibu kwa operesheni ya kulipiza kisasi ya Iran. Salami alisisitiza kwamba Iran inaweza kufanya operesheni kwa kiwango kikubwa zaidi lakini shambulio hilo "lilikuwa na mipaka" kwa kambi za kijeshi za utawala wa Kizayuni, kutoka Miinuko ya Golan hadi Jangwa la Negev, ambazo zilitumiwa katika shambulio la kigaidi kwenye ubalozi mdogo wa Iran jijini Damascus. Iran imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa utakabiliwa na jibu kali ukijaribu kurudisha mapigo baada ya operesheni hiyo ya Iran ya kulipiza kisasi.

3487992

Kishikizo: Ahadi ya Kweli
captcha