IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Kushambuliwa maeneo matakatifu ya Quds kutaibua vita kieneo na Israel itaangamia

22:02 - May 26, 2021
Habari ID: 3473947
TEHRAN (IQNA)-Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa hujuma dhidi ya maeneo matukufu katika mji wa Quds (Jerusalem) inaweza kupelekea kuibuka vita vya kieneo na kuangamizwa utawala huo wa Kizayuni.

Sayyed Hassan Nasrallah ameyasema hayo katika hotuba kwa njia ya televisheni Jumanne usiku, ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tokea harakati za Palestina zitangaze ushindi katika vita na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Ghaza. Aidha ametoa hotuba hiyo kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Mapambano na Ukombozi. Katika siku hii Walebanon huadhimisha ushindi wao dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 2000.

Katika hotuba yake, Sayyid Nasrallah amesema, ushindi wa Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza umewashangaza marafiki na maadui. Ameongeza kuwa utawala wa Israel ulikosea katika mahesabu yake huku akipongeza harakati za mapambano ya Kiislamu au muqawama Palestina kwa kusimama kidete dhidi ya Wazayuni.

Kiongozi wa Hizbullah ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: “Mnapaswa kufahamu kuwa kuudhuru mji wa Quds, Msikiti wa Al Aqsa na matukufu ya mataifa ni tofautu na hujumba zingine mnazotekeleza.” Nasrallah ameonya kuwa, iwapo Israel itauhujumu Msikiti wa al Aqsa na maeneo matakatifu mjini Quds, jibu la jinai hiyo halitatoka tu katika mipaka ya Ghaza bali kutaibuka vita vya kieneo na hatimaye Israel itaangamizwa.

Amesema pale maeneo matakatifu ya Waislamu na Waktristo yanapokabiliwa na hatari, harakati za muqawama haziwezi kukaa kimya na kuwa watazamaji.

Aidha amesema “Oparesheni ya Upanga wa Quds” ya makundi ya muqawama ya Palestina hivi karibuni katika Ukanda wa Ghaza ilikuwa ni pigo kubwa kwa madola ya Kiarabu ambayo yanatekeleza mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel katika fremu ya ‘Muamala wa Karne’.

Israel ilianzisha vita dhidi ya raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na huko Ghaza tangu tarehe 10 mwezi huu wa Mei; na kumalizika tarehe 21 kufuatia ombi la baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni na upatanishi wa baadhi ya pande ajinabi baada ya kushindwa jeshi la utawala huo kukabiliana na wanamuqawama wa Palestina. 

/3474812

captcha