IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Wafanyakazi viwandani Iran hawajakubali kutumiwa vibaya na adui na wanaolitakia mabaya taifa

22:03 - April 29, 2023
Habari ID: 3476930
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, jamii ya wafanyakazi wa viwandani haijakubali kutumiwa vibaya na adui na wanaolitakia mabaya taifa la Iran.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo ​​amehutubia mkutano wa hadhara wa wafanyakazi zaidi ya elfu moja wa viwandani, wanachama wa jumuiya za wafanyakazi hao na maafisa wa Wizara ya Ushirika, Kazi na Ustawi wa Jamii na akaeleza kwamba, katika matukio yote ya maandamano, jamii ya wafanyakazi wa viwandani ilijiwekea mpaka wa kujitenganisha na adui; na sambamba na kusisitiza mshikamano na uungaji mkono wao kwa Mfumo wa utawala, haikuwaruhusu wanaolitakia mabaya taifa la Iran waitumie vibaya kwa manufaa yao mikusanyiko na maadamano ya malalamiko.

Ayatullah Khamenei amesema, kutokuwa na ujasiri wa kupambana na ufisadi wa ndani ndio sababu ya kukosa ushujaa wa kupambana na utumiaji mabavu wa adui wa nje na akaongezea kwa kusema: "kwa kutoa mfano, ikiwa afisa fulani hatakuwa na ujasiri wa kukabiliana na wanaotumia vibaya biashara au mikopo ya benki na akashindwa kuwakabili wadaiwa wakubwa wa benki, hatakuwa na uthubutu pia wa kukabiliana na matakwa ya serikali ya utumiaji mabavu kama Marekani".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja uzalishaji kuwa ndio uti wa mgongo wa nchi na wafanyakazi wa viwandani uti wa mgongo wa uzalishaji na akasema: sehemu muhimu ya kauli mbiu ya mwaka huu ya 'ukuaji wa uzalishaji' inaihusu jamii ya wafanyakazi wa viwandani; hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao katika suala hili inapasa wafanyakazi hao watiwe moyo na wafanye kazi zao bila wasiwasi wowote.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amewataja Mashahidi elfu 14 wa jamii ya wafanyakazi wa viwandani kuwa ni bendera elfu 14 za kujivunia zilizoko mikononi mwa wafanyakazi hao na akaashiria kujitolea mhanga wafanyakazi wa viwandani kwa ajili ya Mapinduzi na Mfumo na akasema: ishara muhimu zaidi ya kujitolea wafanyakazi wa viwandani kwa Mfumo wa Utawala ni mwenendo makini walioonyesha katika miongo hii kadhaa, yaani kuzima njama za magenge mbalimbali mwanzoni mwa Mapinduzi, yaliyokuwa na lengo la kuusambaratisha Mfumo kupitia ufungaji wa karakhana na vilevile kusimama kwao imara na kwa umakini katika kukabiliana na wimbi la propaganda za wenye nia mbaya kutoka nje ya nchi zilizolenga kuigonganisha jamii ya wafanyakazi na Mfumo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwamba, kuwa macho jamii ya wafanyakazi wa viwandani na kutoathiriwa na chokochoko za maajinabi ni "Jihadi Kubwa ya Jamii ya Wafanyakazi" hao na akasisitiza kuwa: "hadi sasa hawajaweza, na baada ya leo pia, kwa msaada na uwezo wa Mwenyezi Mungu hawataweza kuigonganisha jamii ya wafanyakazi wa viwandani na Mfumo"…

/4137090

captcha