IQNA

Zilzala Syria na Uturuki

Waliopoteza maisha katika mitetemeko miwili ya ardhi Uturuki, Syria wapindukia 5,000

19:18 - February 07, 2023
Habari ID: 3476524
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza hali ya dharura katika mikoa 10 iliyotikiswa na mitetemeko miwili ya ardhi ambayo imepelekea zaidi ya watu 5,100 kupoteza maisha nchini Uturuki na Syria.

Siku moja baada ya mitetemeko hiyo kutikisa Uturuki na Syria, waokoaji wanaofanya kazi katika mazingira magumu wanapambana kuwaondoa watu kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Hali ya hewa ya baridi kali imeathiri juhudi za uokozi na upelekaji misaada, na baadhi ya maeneo hayana nishati.

Katika hotuba yake leo, Rais Erdogan amesema mikoa 10 ya nchini Uturuki imeathirika kama eneo la mkasa huo na akatangaza hali ya dharura katika jimbo hilo kwa miezi mitatu. "kwa sasa, tuna vifo vya watu 3,549 na majeruhi 22,168. Faraja yetu kubwa ni kuwa zaidi ya raia wetu 8,000 wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi mpaka sasa."

Erdogan ambaye anakabiliwa na uchaguzi wa kitaifa katika miezi mitatu ijayo amesema serikali inapanga kufungua mahoteli katika mji wa kitalii wa Antalya, katika upande wa magharibi, ili kuwahifadhi kwa muda watu walioathirika na matetemeko hayo. "Tumepokea ahadi za msaada kutoka nchi 70 na mashirika 14 ya kimataifa. Tumezungumza na wakuu 18 wa nchi na serikali ambao" wametupigia simu.

Hii itamruhusu rais na baraza lake la mawaziri kutohitaji idhini ya bunge katika kuweka sheria mpya na kuweka kikomo au kusimamisha haki na uhuru wa watu.

Nchini Syria, idadi ya vifo imefikia watu Zaidi ya 1,600, kwa mujibu wa serikali na idara ya uokozi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kaskazini magharibi.

Timu za uokozi kutoka karibu nchi 30 kote ulimwenguni zinaelekea Uturuki au Syria. Wakati ahadi za msaada zikiendelea kumiminika, Uturuki imesema itayaruhusu tu magari yaliyobeba misaada kuingia katika mikoa iliyoathirika kabisa ya Kahramanmaras, Adiyaman na Hatay ili kuharakisha shughuli za utafutaji na uokozi.

 

Siku ya kiyama

Wakati huo huo, manusura wa matetemeko hayo ya ardhi wametaja hali ngumu na wahka uliowapa wakati wa mitetemeko hiyo wakisema kuwa hawajawahi kukutana na hali kama hiyo licha ya kushuhidia mitetemeko kadhaa ya ardhi katika miaka ya nyuma.

Akisimulia fazaa kubwa iliyotanda kutokana na tetemeko hilo la ardhi, Melissa Salman, 23, mkazi wa mji wa Kahramanmaraş, anasema alidhani Siku ya Kiyama imefika, wakati alipokuwa akizungumza na shirika la habari la AFP, akiwa bado yuko katika hali ya mshtuko. "Hili ni eneo la tetemeko la ardhi, lakini hatujawahi kuona hali kama hii. Tulidhani kwamba ulikuwa mwisho wa dunia", amesema Melissa Salman.

Picha zinazoonyeshwa na televisheni na mitandao ya kijamii, zinatoa muhtasari wa uharibifu mkubwa uliosababishwa na tetemeko hilo la ardhi.

Taarifa zinasema kuwa mtetemeko wa kwanza ulikuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta na umetokea saa kumi na dakika 17 alfajiri ya jana 6 Februari kwa saa za eneo hilo. Kitovu chake kilikuwa ni katika mji wa Gaziantep wa Uturuki ambapo mamia ya majengo yameporomoka. Masaa machache baadaye kulijiri mtetemeko mwingine wa ardhi uliokuwa na ukubwa 7.6 kwenye kipimo cha rishta.

 

Kishikizo: syria uturuki zilzala
captcha