IQNA

Safari ya Raisi nchini Nicaragua; Iran iko mbioni kuimarisha uhusiano na Amerika ya Kusini

14:56 - June 15, 2023
Habari ID: 3477144
Baada ya kumaliza ziara yake rasmi nchini Venezuela, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo amewasili Managua ili kustawisha na kuimarisha uhusiano na Nicaragua. Safari hiyo inafanyiika kwa mwaliko rasmi wa Rais wa nchi hiyo, Daniel Ortega.

Baada ya hafla ya kumkaribisha rasmi iliyotayarishwa na mwenyeji wake, Daniel Ortega, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amehutubia kundi la vijana wa nchi hiyo katika Uwanja wa Uhuru (Managua Revolution Square), akiashiria kusadifiana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Mapinduzi ya Nikaragua na taathira za mapinduzi haya mawili, na amewapongeza mashujaa wa kitaifa wa mapambano dhidi ya ubeberu katika nchi zote mbili.Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja uhusiano kati ya Iran na Nicaragua kuwa ni wa kistratijia na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kustawisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika nyanja zote hususan katika uga wa sayansi na teknolojia.Katika fremu ya sera za kigeni za Iran, suala la kupanua uhusiano na ushirikiano na nchi za Amerika ya Kusini linapewa mazingatio makubwa, na serikali ya Awamu ya 13 ya Iran, kwa mujibu wa kaulimbiu ya siasa zake za mambo ya nje, sambamba na kufanya juhudi za kuimarisha uhusiano na majirani na nchi za kanda wa Magharibi mwa Asia, imetangaza kwamba inataka kupanua uhusiano na nchi zenye mielekeo sawa katika maeneo mbalimbali ya dunia ikiwa ni pamoja na Amerika ya Kusini.

Viongozi wa nchi za Amerika Kusini zikiwemo Venezuela, Cuba na Nicaragua pia wameelezea matumaini yao ya kuimarisha uhusiano wa serikali zao na Iran.

Safari za kidiplomasia na mikutano ya maafisa wa ngazi za juu wa Iran na nchi za Amerika ya Kusini ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na pande hizo mbili kwa ajili ya kuimarisha uhusiano tangu Serikali ya Awamu ya 13 iliposhika hatamu za uongozi. Nicaragua, katika Amerika ya Kusini, ni miongoni mwa nchi ambazo zina uhusiano mzuri na Iran, na viongozi wa nchi hiyo daima wamekuwa wakikaribisha suala la kustawisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu.

Serikali ya Sayyid Ebrahim Raisi, inalipa umuhimu mkubwa eneo la Amerika ya Kusini na kwa mara nyingine tena imefungua faili la ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi na nchi za eneo hilo. Kuhusiana na hilo, mwezi Disemba mwaka 1401, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Nicaragua walitia saini hati ya mapatano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Usafirishaji wa huduma za uhandisi na masuala ya kiufundi, utengenezaji wa dawa, mauzo ya chuma, pamoja na nyanja za sayansi na teknolojia ni miongoni mwa fursa za kiuchumi na kibiashara za Iran nchini Nicaragua. Wakati huo huo, viongozi wa nchi hiyo wana hamu kubwa ya kukidhi mahitaji yao ya nishati kupitia Iran; na kwa kuzingatia ukweli kwamba Nicaragua imewekewa vikwazo na Marekani katika nyanja ya nishati, inaonekana kuwa moja ya fursa nzuri kwa Jamhuri ya Kiislamu ni kupeleka bidhaa za mafuta nchini humo.

Suala la kupanua uhusiano wa pande mbili kati ya Iran na nchi za Amerika ya Kusini, ikiwemo Nicaragua, mbali na manufaa yake ya kiuchumi na kuandaa masoko tofauti ya kibiashara kwa Iran, vilevile ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika mtazamo wa kisiasa na katika kuimarisha mfumo wa kambi nyingi; kwa sababu  ni hatua nyingine ya kutoa kipigo kwa sera za Marekani za kutaka kuitenga Iran na linaimarisha msimamo wa nchi zenye mwelekeo mmoja wa kupinga siasa za kibeberu za Marekani. Hossein Amir Abdollahian

Kuhusiana na suala hilo, Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran pia ameashiria rekodi chanya za mshikamano wa kisiasa baina ya Iran na Nicaragua katika asasi za kimataifa na kusema: Kupinga fikra ya ulimwengu wa kambi moja ni miongoni mwa sifa ya pamoja ya siasa za nchi mbili; na hapana shaka kuwa, kulipa mazingatio eneo la Amerika ya Kusini ni sehemu ya sera ya nje ya Serikali ya Awamu ya 13

Kishikizo: iran raisi
captcha