IQNA

Tunisia yafunga radio na televisheni za Kiislamu

18:45 - July 21, 2015
Habari ID: 3331856
Baraza Kuu la Vyombo vya Habari Tunisia limefunga televisheni na radio kadhaa za Kiislamu nchini humo kwa tuhuma kuwa hazina vibali.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Jumatatu Julai 20 Baraza Kuu la Vyombo vya Habari Tunisia lilitangaza kufunga idadi kadhaa ya radio na televisheni kutokana na kile kilichotajwa ni kuendesha shughuli bila kibali. Vyombo hivyo vya habari vilivyofungwa vilianzishwa baada ya mwamko wa Kiislamu nchini humo mwaka 2011.  Kati ya televisheni zilizofungwa ni al Zaituniya, Tunisna na Radio Qur'an. Vyombo hivyo vya habari vinafungamana na harakati ya Kiislamu ya An Nahdha.
Wakuu wa radio na televisheni hizo wamelalamikia vikali hatua hiyo na kuitaja kuwa inayokiuka uhuru ulioainishwa katika katiba. Wabunge kadhaa wamesema hatua hiyo  imechukuliwa na serikali kwa kisingizio cha hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo kufuatia hujuma ya hivi karibuni ya kigaidi.  Wabunge hao wamesema utawala wa sasa Tunisia unalenga kuirejesha kinyemela nchi hiyo katika zama za dikteta Ben Ali aliyeondolewa madarakni.  Wasimamizi wa vyombo vya habari vilivyopigwa marufuku Tunisia wanasema nchi hiyo sasa haina radio na televisheni zenye kuzingatia maadili na kuzuia kuenea itikadi potofu za misimamo mikali ya kidini. Wanasema kwa mfano katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani televisheni zilizosalia Tunisia zilikuwa zinarusha hewani vipindi vilivyojaa ufuska lakini televisheni na radio za Kiislamu zilikuwa  zinatangaza vipindi vyenye kujaa mafunzo mengi kwa jamii.../mh

3331579

captcha