IQNA

Waislamu duniani waadhmisha siku ya kubaathiwa Mtume Muhammad SAW

20:28 - February 28, 2022
Habari ID: 3474988
TEHRAN (IQNA)- Tarehe 27 Rajab ndiyo siku aliyobaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad bin Abdullah SAW kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu katika njia iliyonyooka. Mtukufu huyo wa daraja alikuwa anapitisha mwaka wa arubaini wa umri wake uliojaa baraka na katika miaka yote hiyo watu walikuwa wakimpongeza kwa ubora wa tabia na uaminifu wake.

Pango la Hiraa lilikuwa mahala ambapo Mohammad alikuwa akitulia kiroho. Katika sehemu hii alikuwa akipitisha baadhi ya siku akiwa amezama katika ibada na kutafakari. Kila alipokuwa akimaliza ibada zake hapo alikuwa akielekea katika Kaaba na kutufu.Wakati Mtume SAW alipokaribia miaka 40, alikithirisha ibada na itikafu. Sijda zake zilikuwa ndefu zaidi, minong'ono yake na Mola wake iliongezeka na kuzama katika kina kirefu zaidi wakati wa kutafakari. Kwa kweli alikuwa na hali tafauti kabisa kimaanawi. Mahaba na mapenzi ya Mohammad SAW kwa Mwenyezi Mungu yalikuwa makubwa sana kiasi cha yeye kustahiki kupokea Wahyi.

'Soma kwa Jina la Mola Wako Mlezi aliyeumba'

Mohammad SAW katika hizo lahadha zilizojaa nuru, alisikia sauti wakati akiwa amezama katika hali ya kumuabudu Mola wake. Sauti hiyo ilimuamrisha asome. Jibril, Malaika wa Wahyi alikuwa ameamurishwa kumpa Mohammad ujumbe muhimu. Alimwambia, 'Ewe Mohammad! Soma.' Mohammad ambaye alikuwa hajui kusoma, huku akiwa ameshangaa sana aliuliza: ‘Nisome nini? Sijui kusoma. Kwa mara nyingine Jibril alirudia na kusema: 'Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.' (Surat al A'laq aya ya 1-5)Mohammad hapo alifahamu kuwa alikuwa ameteuliwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu kuwaongoza wanaadamu kwa kueneza ujumbe Wake. Hivi sasa imepita zaidi ya miaka 1400 tokea lijiri tukio hilo ambalo lilikuwa nukta adhimu katika historia ya mwanaadamu. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kubaathiwa Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW na tunawakarisbisha kusikia machache tuliyowaandalia kwa munasaba huu.Mwenyezi Mungu SWT katika aya ya pili ya Surat al Jumua anasema: Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.Nukta ya kwanza ya ayah hii inahusu kusoma aya za Mwenyezi Mungu. Kwa kusoma aya za Mwenyezi Mungu na kuwajulisha watu kuhusu aya hizi, Mtume wa Uislamu SAW alikuwa anaandaa mazingira ya kuwafundisha.Emile Dermenghem, mtaalamu wa masuala ya Mashariki na mwandishi Mfaransa anasema hivi kuhusu nukta hii: ‘Sheria muhimu zaidi ya mabadiliko na mafundisho ni ule ukweli ambao ulikuja kwa jina la Wahyi na hatua kwa hatua kumteremkia Mohammad SAW na leo miongoni mwa wanaadamu jina lake ni Qur'ani

.'Mohammad SAW, mkamilishaji maadili mema;

Moja kati ya hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na Mtume wa Uislamu SAW ni kuwalea wanaadamu.Malezi haya yanamaanisha kuandaliwa mazingira ya kunawirisha vipawa vya mwanaadamu katika njia inayofaa.Jitihada zote za Mtume SAW zilielekezwa katika kuandaa mazingira ya uhusiano bora baina ya mwanaadamu na Allah SWT na halikadhalika na wanaadamu wenzake.Ili kufikia lengo hili, kulikuwa na ulazima wa kuisafisha nafsi ya mwanaadamu ili kuitayarisha kupokea ukweli bora zaidi.Katika Qur'ani Tukufu amali hii imetajwa kuwa ni Tazkiyatun Nafs kwa maana ya kulea vizuri na utakasaji unaojumuisha kuwa mtakasifu kwa mtazamo wa kiitikadi, kiakhlaqi na kitabia.Umuhimu wa akhlaqi au maadili mema na Tazkiyatun Nafs ni mambo ambayo hayajafichika kwa yeyote na jamii mbali mbali zinayahitaji hayo. Hii ni kwa sababu njia ya kuokoka kutoka upotofu, ufisadi, ujahili, vita na umwagaji damu ni kupitia kujipamba kwa thamani na maadili bora.Mtume Mtukufu SAW alisema lengo la kubaathiwa na kutumwa kwake ni kukamilisha maadili mema: "Hakika si jambo jingine bali nimetumwa ili kukamilisha maadili mema."Naam, Mtume SAW alikuja kwa ajili ya kulea na kukamilisha maadili na kutakasa moyo wa mwanaadamu sambamba na kukuza elimu na ujuzi wake. Kwa kutumia mabawa hayo mawili ya maadili bora na elimu, mwanaadamu huweza kupaa na kupata saada katika njia ya kuelekea kwa Allah SWT na hivyo kufika katika nafasi ya juu anayostahiki. Kwa hakika katika Qur'ani Tukufu suala la elimu au mafunzo limetajwa sambamba na utakasaji nafsi na hili linaonyesha ni kwa kiwango gani kila moja ya nukta hizo huathiri nyingine.Hakuna shaka kuwa katika kila uga hasa katika masuala ya kiakhlaqi, wanaadamu wanahitaji kigezo bora na kilichokamilika.

Mohammad SAW, kigezo bora zaidi

Mwenyezi Mungu SWT amewaonyesha wanaadamu kigezo bora zaidi.Amewaonyesha mwanadamu yule yule ambaye ameteuliwa kuwaongoza wanaadamu wenzake kuelekea katika njia ya Mwenyezi Mungu na ambaye binafsi alikuwa kigezo bora zaidi cha maadili na vitendo. Katika Qur'ani Tukufu tunasoma hivi:‘Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ....'Surat al Ah'zab Aya ya 21Kwa mujibu wa aya hii, Mtume SAW sambamba na kubainisha nadharia ya maadili, ili kakamilisha maadili bora katika jamii, yeye mwenyewe alitekeleza kivitendo maadili mema. Kuhusiana na hili, Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu Aya ya nne Surat al Qalam amemhutubu Mtume SAW kwa kusema, ‘Na hakika wewe una tabia tukufu.'Taathira hii kubwa ya kimaadili ya Mtume SAW ndiyo iliyompelekea kuwakusanya Waarabu Mabedoui wa zama za Jahiliya na kuwahubiria dini ili kuwaondoa katika dimbwi la ujalili na kuwapeleka katika njia iliyojaa nuru ya Mwenyezi Mungu.Lengo kuu la kubaathiwa Mtume SAW na Mitume wote ni kuongoza na kutakasa nafsi za wanaadamu wote.Mitume wote walitumwa katika mhimili wa kumuamini Mwenyezi Mungu na hawakuwa na lengo lingine ila kuwaongoza wanaadamu. Kwa hivyo Mitume wote walifuata njia moja. Kile kilichotofautiana ni kuhusu masuala ya dini na sheria. Wanaadamu katika vipindi vyote vya historia wamekuwa wakitegemea juhudi za Mitume wa Mwenyezi Mungu kwani bila wao, wangefuata mkondo wa waliopotea.Mtume wa Mwisho Mohammad SAW, ambaye alibeba ujumbe wa mwisho wa Allah na kuleta rehma na dini kamilifu zaidi duniani, alibaathiwa ili kuwaokoa wanaadamu wote.Mtume Mohammad SAW kwa kusoma aya za Wahyi na kuweka wazi njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu, aliweza kuongoza nyoyo za wanaadamu kuelekea katika nuru ya uongofu. Hili ndilo lengo la juu la kubaathiwa Mtukufu huyo. Kwa hivyo malezi bora na kuwaongoza wanaadamu katika njia ya haki sambamba na kutenganisha haki na batili na kheri na shari ni jukumu muhimu la mitume hasa Mtume Mtukufu SAW. Hili ni lengo ambalo limesisitizwa mara kadhaa katika Qur'ani Tukufu. Katika aya ya 11 ya Surat al Mujaadalah Allah SWT anasema: ... Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa ilimu daraja za juu....Kwa hivyo, lengo muhimu na la juu la kubaathiwa Mtume Mtukufu wa Uislamu ni Tazkiyatun Nafs au kutakasa nafsi za watu na kuondoa mafungamano ya kimaada katika nyoyo za watu na kuwaongoza katika ubora wa kimaanawi.

Dunia inahitaji mafundisho ya Mohammad SAW

Wakati tunapoangalia hali mbaya ya hivi sasa duniani tunahisi kuwa Bwana Mtume aliteuliwa kwa ajili ya zama hizi na malengo na mafunzo yake ni yenye kumuongoza mwanaadamu anayekumbwa na masaibu katika karne ya 21.Maadili bora na umaanawi ni johari zilizopotea za mwanaadamu katika zama hizi na hayo mawili yaliweza kuwasilishwa na Mtume SAW kwa njia ya juu na bora zaidi kwa wanaadamu wote. Ni kwa sababu hii ndio hivi sasa tunashuhudia namna siku hadi siku watu wanavutiwa na dini ya Mtume Mohammad SAW ambayo ujumbe wake mkubwa ulianzia katika Pango la Hiraa ili kuwaongoza wanaadamu katika njia kamilifu iliyojaa nuru. Sala na Salamu za Mwenyezi Mungu zimfikie Mtume (SAW) na Kizazi chake Kitoharifu (AS).

 

captcha