IQNA

Mahakama ya Uturuki kutangaza uamuzi kuhusu Hagia Sophia wiki mbili zijazo

14:12 - July 03, 2020
Habari ID: 3472926
TEHRAN (IQNA) – Mahakama ya Uturuki siku ya Alhamisi ilisikiliza kesi kuhusu Jumba la Makumbusho la Hagia Sophia mjini Istanbul kurejeshwa katika hadhi yake ya msikiti.

Kwa mujibu wa taarifa mahakama hiyo inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi hiyo katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amependekeza kuwa Jumba la Makumbusho la Hagia Sophia mjini Istanbul ligeuzwe matumizi na kurejea katika hadhi yake ya msikiti, Jengo hilo limesajiliwa na UNESCO kama turathi ya kimataifa na lilijengwa mwaka 537 Miladia (CE) na lilipata umaarufu kutokana na kuba lake adhimu na wakati huo lilikuwa jengo kubwa zaidi duniani. Tokea mwaka 537 hadi 1453 lilikuwa ni Kanisa la Mashariki la Kiothodoxi na makao makuu ya Kasisi Mkuu wa Constantinople. Kwa muda mfupi, kati yaani kati ya mwaka 1204 hadi 1261, jengo hilo liligeuzwa na Wapiganaji wa Nne wa Msalaba kuwa Kanisa Katoliki. Wakati watawala wa silsila ya  Wauthmaniya (Ottomans) walipouteka mji huo, mnamo mwaka 1453 Fatih Sultan Mehmet aliagiza jengo la Hagia Sophia litumike kama msikiti. Hadhi hiyo ya Hagia Sophia kama msikiti iliendelea kwa muda wa miaka 482 hadi mwaka 1935 wakati muasisi wa Jamhuri ya Uturuki, Mustafa Kemal Ataturk alipoagiza ligeuzwe na kuwa jengo la makumbusho.

Kesi iliyofikishwa mahakamani inahusu uhalali wa uamuzi wa Ataturk kugeuza msikiti huo kuwa jengo la makumbush. “Tunataraji kuwa mahakama itatoa hukumu kuwa kugeuzwa  Hagia Sophia kuwa Jengo la Makumbusho kwa muda wa miaka 86 ni jambo ambalo limewasikitisha na kuwaumiza watu wa Uturuki,” amesema Selman Karaman, wakili wa jumuiya ambayo imefikisha kesi hiyo mahakamani.

Uchunguzi wa maoni ambao umefanyika hivi karibuni umeonysha kuwa, Zaidi ya asilimia 73 ya watu wa Uturuki wanataka Jumba la Makumbusho la Hagia Sophia mjini Istanbul lirejee katika hadhi yake ya msikiti.

3471864

captcha