IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Rwanda yafanyika

14:21 - June 25, 2018
Habari ID: 3471572
TEHRAN (IQNA)- Mashindano ya 7 Kimataifa ya Kuhifadhi Qur'ani ya Rwanda yamemalizika Jumamosi ambapo mshindi alikuwa Maazu Ibrahim Muadh wa Niger ambaye aliwashinda washiriki 42 kutoka nchi 17 za Afrika.

Sherehe za kufunga mashindano hayo zilifanyika katika Uwanja wa Mpira wa Nyamirambo mjini Kigali ambapo mwenyeji Rwanda ilikuwa na washiriki 22.

Taarifa zinasema Muadh alipata pointi 99.6 pamoja na zawadi ya fedha taslimu  faranga ya Rwanda (Rfw) milioni moja pamoja na tiketi ya Hija.

Washiriki 19 walifika katika fainali ya mashindano hayo ambapo hatimaye watano bora walitangazwa.

Nafasi ya pili katika mashindano hayo ilichukuliwa na Ali Abdi Nasir wa Kenya ambaye alipata pointi 98.70 na kutunukiwa zawadi ya fedha taslimu Rfw500,000.

Akiwahutubia maelfu ya Waislamu waliofika katika siku ya mwisho ya mashindano hayo ya Qur'ani, Mufti wa Rwanda Sheikh Salim Hitimana alisema Mwislamu anapaswa kuwa na uzalendo, mapenzi sambamba na kuleta umoja na kuunga mkono usalama.

Amesema mashindano hayo ya kuhifadhi Qur'ani yanalenga kuhimiza kizazi cha vijana kusoma na kujifunza Qur'ani kwa ajili ya kuleta mabadiliko na ustawi wa thamani za kidini.

3466156

captcha