IQNA

Wayemen na jinamizi la mauti kutokana mabomu ya Saudia, magonjwa, njaa

11:36 - December 15, 2017
Habari ID: 3471310
TEHRAN (IQNA)- Wananchi wa Yemen wanakumbwa na jinamizi la mauti ambalo lilianza wakati Saudi Arabia, kwa himaya ya Marekani na Israel, ilianzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo Machi 2015.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema katika ripoti yake mpya kwamba, raia 34 wa Yemen wamefariki dunia baada ya kuambukizwa ugonjwa wa dondakoo (diphtheria) ambao husababisha kupumua kwa shida. Kwa hakika maisha ya wananchi wa Yemen yamegeuka na kuwa simulizi chungu iliyojaa simanzi na majonzi. Takwimu za mgogoro wa kibinadamu wa Yemen zilizotolewa wiki iliyopita na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa zinabainisha wazi kisa cha majonzi cha wananchi wa Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hadi kufikia Oktoba mwaka huu takribani watu 8,800 wa Yemen walikuwa wameuawa na wengine zaidi ya elfu 51 kujeruhiwa. Aidha ripoti hiyo inaeleza kwamba,  raia milioni 22.2 wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu wanahitajia misaada ya kibinadamu. Kadhalika ripoti hiyo inasema kwamba, raia milioni 17.8 wa nchi hiyo wanakabiliwa na tatizo la usalama wa chakula. 

Kipindupindu

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, raia milioni tatu wamekuwa wakimbizi ndani ya Yemen na kwamba watu milioni 16 wa nchi hiyo hawana uwezo wa kupata maji safi na salama ya kunywa. Kuanzia Aprili hadi Novemba 13 mwaka huu, kumeshuhudiwa zaidi ya kesi 900 za ugonjwa wa kipindupindu ambapo zaidi ya watu 2200 wameshapoteza maisha yao kwa maradhi hayo.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, wananchi wa Yemen wanakabiliwa na mauti na hawana njia ya kukimbilia. Kuangukiwa na mabomu, baa la njaa, waba, maji yasiyo salama, kutokuweko uangalizi wa kiafya na hatimaye ugonjwa wa dondakoo ni mambo ambayo kwa hakika yanawasukuma wananchi wa nchi hiyo katika makucha kifo. Hali hiyo mbaya haiishii katika baadhi ya maeneo tu ya Yemen, bali maeneo yote ya nchi hiyo yanashuhudia maafa haya.

Dondakoo

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) maradhi ya dondakoo yanashuhudiwa katika mikoa 15 na katika miji zaidi ya 64 ya nchi hiyo. Katika hali hiyo, picha za watoto wadogo wa Yemen wanaogaragara wakipania kubakia hai, ndizo zenye kuumiza zaidi kuliko kitu kingine chochote.

Ujahili wa Saudia

Ujahili wa kisiasa wa utawala wa Aal Saud ndio uliwafanya wananchi wa Yemen wakumbwe na masaibu haya machungu na ya kuhuzunisha. Katika kila aina ya kifo kinachowakabili wananchi wa Yemen, kunashuhudiwa athari za jinai za utawala wa Aal Saud. Mabomu yanayorushwa kila siku na ndege za kivita za Saudia na washirika wake, magonjwa, njaa na kutokuweko uangalizi wa kiafya ni mambo ambayo kwa hakika yamewafanya wananchi wa Yemen wawe katika ukingo wa kifo.

Yemen ni 'Vietnam ya Saudia'

Hali ya Yemen ambayo imepewa jina la 'Vietnam ya Saudia' imekuwa mbaya kiasi kwamba, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaonekana kuachana na dola za mafuta za Saudia kwani ameikosoa wazi wazi Saudia kuhusiana na hujuma na vita vyake huko Yemen.

Hata serikali ya Marekani imedai kusikitishwa na jinai hizo za Saudia  lakini ukweli ni kuwa kutokana na jinai za Aal Saud, sasa Wayemen wanakabiliwa na jinamizi la mauti kila waendapo katika nchi yao na bila shaka Marekani na utawala haramu wa Israel ni washirika wakuu wa jinai hizo.

3464693

captcha